Tanzania yapokea mkopo wa bilioni 517 za uboreshaji reli ya kati

0
51

Tanzania imepata mkopo wa dola za Marekani milioni 200 (takriban bilioni 517) kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Benki ya Dunia (IDA), kwa ajili ya awamu ya pili ya Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya kati (TIRP-2).

Mkopo huo mpya unafuatia dola za Marekani milioni 270 zilizokopeshwa na IDA kwa awamu ya kwanza iliyokamilika Septemba 2022, ambapo fedha hizo zilihusisha mambo mbalimbali ikiwemo ukarabati wa njia na madaraja, kuongeza uwezo wa kubeba mzigo toka chini ya tani 13.5 za uzito wa ekseli hadi tani 18.5 na kukarabati vituo vya kati katika Bandari ya Dar es Salaam, Ilala na Isaka.

Rais atoa tani 189 za mbegu kwa wakulima walioathirika na mafuriko Kilombero

Katika awamu hii, fedha hizo zitatumika kugharamia usalama wa reli dhidi ya majanga ya asili, ustahimilivu wa hali ya hewa na uboreshaji wa ufanisi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Isaka yenye urefu wa kilomita 970.

Aidha, IDA inasema mbali na wanufaika wa moja kwa moja 900,000 wa mradi, mradi huo, pia utakuwa na matokeo chanya kwa takribani watu milioni 3.5, sawa na asilimia 5 ya watu wote wa Tanzania. Hii ni pamoja na abiria na wanaosafirisha mizigo, wakazi kando ya reli, wafanyabiashara, na jamii katika eneo la kukusanya maji la Kinyasungwe.

Send this to a friend