Tanzania yapokea msaada wa TZS bilioni 78.6 kutoka Ujerumani

0
150

Tanzania na Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) zimesaini mikataba mitatu ya misaada yenye thamani ya Euro milioni 25.68 [sawa na TZS. bilioni 78.58] kwa ajili ya miradi ya maji na maliasili.

Mikataba hiyo imesainiwa katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na kwa upande wa Ujerumani imesainiwa na Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Manuel Muller na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) anaesimamia nchi za Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya, Christoph Tiskens.

Dkt. Mwamba amesema mikataba iliyosainiwa ni kwa ajili ya mradi wa programu ya ufadhili wa miradi ya maji inayotegemea matokeo kwa kiasi cha Euro milini 10 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 30.6.

Mkataba mwingine ni wa fedha za kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya mradi wa ustahimilivu wa tabia nchi (Climate Resilient Towns project) kwa kiasi cha shilingi bilioni 2.08.

Mkataba wa tatu ni wa utekelezaji wa mradi wa Uhifadhi wa Maliasili unaojulikana kama Project for Sustainable Development of Protected Areas kwa kiasi cha Euro milioni 15 sawa na TZS bilioni 45.9.

Lengo la miradi hiyo imeelezwa kuwa ni kutoa motisha kwa mamlaka za maji hapa nchini kukopa kutoka Benki za Kibiashara kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji ili kuboresha huduma na kuongeza mapato.

Send this to a friend