Serikali imepokea Dola za Kimarekani milioni 602, sawa na trilioni 1.4 za Kitanzania kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi mwaka 2026.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu wakati akifungua Mkutano wa mkakati wa utekelezaji wa fedha hizo ambapo amesema fedha zilizopokelewa zimetokana na jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu katika kuboresha huduma za afya ili ziweze kuwafikia wananchi katika maeneo yao bila kikwazo.
“Tunatakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji na kuongeza uwajibikaji kwa lengo la kuboresha hali ya utoaji wa huduma za Afya nchini. Ili kufikia malengo haya, wote tunao wajibu wa kusimamia na kutekeleza ipasavyo mipango tuliyojiwekea na kuwezesha shughuli zote za mradi ambazo zimepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha mwaka 2024-2026 zinakamilika kwa asilimia mia moja,” Amesisitiza.
Naye, Mwakilishi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Subisya Kabuje, amesema Wizara yao imekuwa mnufaika mkubwa wa fedha za Mfuko wa Dunia ambapo katika kipindi cha awamu ya sita TAMISEMI ilipokea shilingi Bilioni 39.9 zilizofanikisha ukamilishaji wa mfumo wa taarifa za afya wa GoTHOMIS ambao umekuwa kichocheo kikubwa katika kusimamia huduma za afya kwenye ngazi za Mikoa na Vituo vya afya.