Tanzania yaruhusu raia wa nchi za SADC na EAC kuwekeza kwenye dhamana za Serikali

0
22

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kanuni mpya za fedha za kigeni za mwaka 2022 zilizotungwa zinaruhusu wakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuwekeza katika dhamana za Serikali za muda mfupi na mrefu.

Aidha, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Florens Luoga imeeleza kuwa kanuni zilizotungwa zinaruhusu mkazi wa Tanzania kuwekeza katika nchi za wanachama wa jumuiya hiyo.

Awali, Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ilikutana Juni 6, mwaka huu kutathmini mwenendo wa sera ya fedha mwezi Machi na Aprili 2022, pamoja na hali ya sasa ya uchumi wa kimataifa na uchumi wa ndani.

MPC imesema tangu mkutano wake wa mwisho mwezi Machi, uchumi wa dunia uliendelea kukabiliana na changamoto za kupanda kwa mfumuko wa bei kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19 na changamoto za ugavi unaochangiwa na vita nchini Ukraine pamoja na vikwazo kwa Urusi, hivyo zimezorotesha jitihada za kuinua shughuli za kiuchumi za kimataifa na za ndani.

Pia kamati hiyo imesema shughuli za kiuchumi za ndani zilikua kwa 4.9%, ikilinganishwa na lengo la asilimia 5 Tanzania Bara, na kukua kwa asilimia 5.1 Zanzibar ikilinganishwa na lengo la asilimia 5.2, mikopo ya sekta binafsi imeongezeka kwa asilimi 13.4, sawa na lengo la angalau asilimi 10.6 na mwenendo wa shughuli za fedha ulikuwa kwenye mwelekeo mzuri, ambapo ukusanyaji wa mapato uliimarika sambamba na shughuli za kiuchumi na ulipaji kodi kwa hiari.

Send this to a friend