Tanzania yashika nafasi ya 4 Afrika kwenye usalama wa anga

0
76

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania imeshika nafasi ya nne barani Afrika kwenye masuala ya usalama wa anga kwa kupata alama 86.7 ikitanguliwa na Nigeria, Kenya na Ivory Coast katika ukaguzi uliofanywa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) Mei, 2023.

Akizungumza wakati akifungua maadhimisho ya miaka 20 ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) jijini Dar es Salaam, amesema ukaguzi huo umefanyika katika viwanja vya ndege vya KIA, Zanzibar na Julius Nyerere ambapo amesema Tanzania imeongeza uwezo wa udhibiti wa sekta ndogo ya usafiri wa anga nchini kwa viwango vya kimataifa.

“Kupitia kaguzi za Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO), sekta ndogo ya usafiri wa anga nchini, imeongeza uwezo kutoka asilimia 37.8 mwaka 2013 hadi asilimia 69.04 mwaka 2019. Kutokana na ufaulu huo, ICAO imetoa ufadhili wa dola za Marekani milioni 1 ambazo zilitumika kwenye mradi wa kuendelea kuboresha uwezo wa usimamizi wa anga letu,” amesema.

Waziri Mkuu ametaja mafanikio mengine kuwa ni ongezeko la mchango wa sekta ya uchukuzi katika pato la taifa huku akibainisha kuwa katika utekelezaji wa mpango wa pili wa taifa wa maendeleo, sekta hiyo ilichangia asilimia 8.2 ya pato la taifa kwa mwaka 2022, na kwamba jitihada mbalimbali za serikali katika kuboresha sekta hiyo zimesaidia kuongeza idadi ya abiria na mizigo inayosafirishwa nchini.

Utafiti: Dar yaongoza kwa wanawake kuharibikiwa mimba

Naye Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema anaamini kuwa ukifanyika ukaguzi mwingine, Tanzania itafikisha alama zaidi ya 90, huku akieleza kuwa serikali inaendelea na ufungaji wa mitambo ya kuongoza ndege kwenye viwanja vya ndege vilivyoko Pemba, KIA, Mwanza, Songwe na Arusha.

Send this to a friend