Tanzania yashika namba 4 Afrika kwa kuvutia uwekezaji sekta ya madini

0
1

Tanzania imeshika nafasi ya nne barani Afrika katika mvuto wa uwekezaji kwenye sekta ya madini, kulingana na tathmini ya kimataifa ya mwaka 2025 iliyotolewa na Fraser Institute.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya utafiti wa kampuni za uchimbaji madini, Tanzania imepata nafasi hiyo katika kielezo cha Investment Attractiveness Index (IAI), ikitanguliwa na Botswana, Morocco na Zambia.

Ripoti hiyo inaonyesha pia kuwa kimataifa Tanzania imeshika nafasi ya 34 kati ya maeneo 68 yaliyotathminiwa duniani, ikiwa ni miongoni mwa maeneo yanayozidi kuvutia wawekezaji katika utafiti na maendeleo ya miradi ya madini.

Kwa mujibu wa tathmini hiyo, alama ya Tanzania katika kielezo cha IAI imeendelea kupanda ambapo imefikia 68.04 mwaka 2025, ikilinganishwa na 62.75 mwaka 2024 na 46.38 mwaka 2023, hali inayodhihirisha kuongezeka kwa uaminifu wa wawekezaji katika sekta ya madini nchini.

Kielezo cha IAI hupima mvuto wa uwekezaji kwa kuzingatia vipengele viwili vikuu: uwezo wa kijiolojia wa rasilimali madini na mazingira ya sera na biashara. Katika tathmini hiyo, asilimia 60 ya alama hutokana na uwezo wa rasilimali madini, huku asilimia 40 ikitokana na mfumo wa sera na mazingira ya biashara.

Send this to a friend