![](https://swahilitimes.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250213-WA0024-905x613.jpg)
Tanzania imeshinda nafasi mbili zilizokuwa zikigombewa katika uchaguzi wa Taasisi za Umoja wa Afrika ambazo ni nafasi ya Mjumbe wa Tume ya Umoja wa Afrika inayohusiana na sheria za kimataifa, iliyokuwa ikigombewa na Profesa Kennedy Gastorn na nafasi ya Mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa Umoja wa Afrika dhidi ya rushwa iliyokuwa ikigombewa na Benjamin Kapera.
Profesa Gaston ameshinda kura 45 kati ya kura 48, na Kapera ameshinda kura 33 kati ya kura 48 zilizopigwa katika kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika.
Wajumbe hao walioshinda watawakilisha Kanda ya Mashariki wakiungana na wajumbe wengine kutoka Kanda za Magharibi, Kaskazini, Kusini na Kati katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo.
Nafasi ya Ujumbe wa Tume ya Sheria za Kimataifa ni miaka mitano, huku nafasi ya Ujumbe wa Bodi wa masuala ya Rushwa ni miaka sita.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki, Thabit Kombo ametumia fursa ya kikao hicho kumnadi mgombea wa nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi.