
Serikali imetangaza kuwa itazuia uingizaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini kufikia siku ya Jumatano ijayo, iwapo nchi hizo hazitabadilisha msimamo wao wa kuweka vikwazo dhidi ya bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.
Hatua hiyo inafuatia taarifa rasmi kuwa Serikali ya Malawi imezuia uingizwaji wa bidhaa kadhaa za kilimo kutoka Tanzania, ikiwemo unga, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi, hatua iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania wanaosafirisha bidhaa hizo.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema licha ya jitihada za kidiplomasia na mawasiliano na Waziri wa Kilimo wa Malawi, bado hakuna majibu yoyote rasmi, na hivyo serikali inalazimika kuchukua hatua za kulinda maslahi ya wakulima na wafanyabiashara wa ndani.
“Ni vyema ifahamike kuwa kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio. Hali hii inafanana na changamoto tulizopitia kwa zaidi ya miaka kumi katika kufungua soko la parachichi, hadi pale tulipoamua kuchukua hatua za kulinda maslahi ya nchi yetu,” amesema Waziri Bashe
Katika taarifa hiyo, Waziri Bashe amebainisha yafuatayo:
- Kuanzia Jumatano ijayo, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka nchi hizo mbili.
- Mizigo ya bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini haitaruhusiwa kupita ndani ya mipaka ya Tanzania, kuelekea bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote, hadi zuio hilo litakapoondolewa.
- Usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi utasitishwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda maslahi ya wakulima na wafanyabiashara wa Kitanzania.
Aidha, wafanyabiashara wote wametakiwa kusitisha mara moja upakiaji wa bidhaa zinazoelekea Malawi hadi itakapotolewa taarifa mpya.