
Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden umetangaza fursa za ufadhili kamili wa masomo ya Shahada ya Uzamili unaotolewa na Taasisi ya Sweden (Swedish Institute – SI) kwa Watanzania, katika zaidi ya programu 400 za masomo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa ufadhili huo unatolewa katika nyanja za utawala, afya ya umma, ujasiriamali na ubunifu, sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati na fani nyinginezo.
“Ufadhili huu ni wa malipo ya ada, posho ya kila mwezi pamoja na gharama za usafiri. Ubalozi unawahamasisha Watanzania wenye sifa stahiki kuomba ufadhili huu,” imeeleza taarifa.
Sifa za mwombaji zimetajwa kuwa ni; awe raia wa Tanzania, awe ameomba au anaomba programu ya Shahada ya Uzamili inayostahiki kwa udhamini wa SI, awe tayari kulipa ada ya maombi ya masomo kupitia mfumo wa udahili wa vyuo vikuu, awe na uzoefu wa kazi unaothibitika, awe na uzoefu wa uongozi kutoka kwa mwajiri wa sasa au wa awali au kupitia Shirika katika asasi za kiraia.
Aidha, mwombaji anapaswa kutembelea tovuti rasmi ya udahili wa vyuo vikuu vya Sweden kupitia https://www.universityadmissions.se/intl/start. Tarehe ya mwisho wa maombi ni Januari 15, 2026.






