Tanzania yatenga hekta 20 Bandari Kavu ya Kwala kwa ajili ya Zambia

0
22

Tanzania imetenga eneo la hekta 20 katika Bandari Kavu ya Kwala maalum kwa ajili ya mizigo inayopita nchini Tanzania kwenda nchini Zambia ili kuongeza ufanisi na kupunguza msongamano, pamoja na kuoandoa ucheleweshaji wa mizigo.

Hayo yamesemwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia katika maadhimisho ya miaka 59 ya uhuru wa nchi hiyo akitoa kama zawadi kwa wananchi wa Zambia ili kupunguza gharama za kufanya biashara miongoni mwa nchi hizo mbili.

“Kutokana na azma yetu ya kuendeleza biashara kati ya nchi zetu mbili, serikali yangu imefanya uamuzi wa kutenga hekta 20 katika Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani kwa ajili ya mizigo ya Zambia,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa Tanzania inaendelea na maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam na kuisihi jumuiya ya wafanyabiashara wa Zambia kuitumia kwani maboresho hayo yataongeza ufanisi na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kwa kasi na kwa wakati.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania na Zambia zitaendelea kuweka mazingira mazuri ili kuhakikisha usafirishaji wa bidhaa na watu unakuwa huru, akiongeza kuwa yeye pamoja na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema ni waumini wa kuwawezesha wananchi katika maendeleo ya kiuchumi.

Naye, Rais Hakainde amesema ushirikiano uliopo baina ya Tanzaia na Zambia unapaswa kuendelea kuimarishwa kwa ajili ya manufaa ya watu wake huku akihimiza bara la Afrika kutunza amani na kujiepusha na vita.

Send this to a friend