Kikosi cha Tembo Warriors leo Oktoba 5, 2022 kimeendelea kuishangaza dunia kwa kuibamiza vibaya timu kali ya Japan katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa ulemavu yanayoendelea nchini Uturuki.
Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini, Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu wake Dkt. Hassan Abbasi wameongoza kutoa hamasa na mikakati ya ushindi huo wakiungana na watanzania waishio Uturuki.
Akizungumza kwa baada ya ushindi huo, Waziri Mchengerwa amesema timu hiyo imeonyesha uzalendo mkubwa kwa Taifa lao kilichobaki ni kumalizia kutwaa kombe Kwa kuwa wanauwezo mkubwa wa kurejesha kombe hilo nyumbani.
Aidha, amefafanua kuwa, Serikali ya Tanzania ipo pamoja na timu hiyo katika kila hatua na ndio maana Rais ameridhia kuzigharimia timu hiyo kwa kila kitu ili iendelee kufanya vizuri.
Pia, ameendelea kusisitiza kuwa ahadi zawadi nono kwa timu hiyo ikiwemo shilingi milioni 40 endapo watafuzu robo fainali, shilingi milioni 80 wakifuzu kucheza nusu fainali na shilingi milioni 100 wakifanikiwa kufuzu fainali za michuano hiyo ipo palepale.
Amewataka wachezaji kuendelea kuzingatia nidhamu, umoja na kumtanguliza Mungu na kusema kuwa Serikali ipo kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.