Tanzania yatoa kibali cha kusafirisha makinikia nje ya nchi

0
48

Miaka mitatu tangu ilipoweka zuio, Serikali ya Tanzania imetoa kibali cha kusafirisha kwenda nje ya nchi makontena 277 yenye mchanga (makinikia) wa dhahabu na shaba.

Makontena hayo yamekuwa yakishikiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam tangu mwaka 2017, yakisubiri majadiliano katika ya serikali na kampuni ya Barrick Gold-Corp. ya Canada.

Akinukuliwa na Gazeti la Mwananchi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema kuwa kibali kimetolewa kwa Twiga Minerals kufuatia Barrick Gold kulipa kodi zote zenye thamani ya TZS 21.1 bilioni.

“Kwa ufupi, kibali cha kusafirisha nje kimetolewa. Kodi zote zilikuwa zimelipwa hadi Aprili. Uamuzi wa lini kusafirisha makinikia unabaki kwa kampuni (Twiga) yenyewe,” amesema Prof. Msanjila.

Kibali hicho kimetolewa ikiwa ni miezi minne tangu serikali na Barrick Gold zilipotangaza zimesaini makubalino ambayo yataifanya Tanzania kunufaikia na migodi mitatu ya kampuni hiyo iliyopo nchini.

Miongoni mwa mambo yaliyoridhiwa na pande hizo mbili ni Barrick Gold kulipa malimbikizo ya kodi yenye thamani ya TZS 694 bilioni, kuondolewa zuio la kusafirisha makinikia nje ya nchi pamoja na kunufaika kwa pamoja na migodi iliyopo nchini

Awali, kamati ya uchunguzi iliyoundwa na Rais Dkt Magufuli mwaka 2017 kuchunguza makontena hayo ilitoa orodha iliyoonesha uwepo wa madini tofauti tofauti kwenye mchanga huo ambayo thamani yake ni TZS 829.4 bilioni, tofauti ya takwimu zilizotolewa na Acacia Mining.

Send this to a friend