Tanzania yavuna bilioni 12 kutokana na Kombe la Dunia Qatar

0
41

Tanzania imenufaika na fainali za Kombe la Dunia la FIFA nchini Qatar kutokana na kuongezeka kwa mauzo ya nyama katika nchini Qatar katika muda wote wa mashindano hayo.

Qatar ndiyo mwagizaji mkubwa wa nyama kutoka Tanzania hasa nyama ya mbuzi ikifuatiwa na Oman, Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia na Bahrain.
Maeneo mengine yanayoongoza ni Kenya, Togo, Kuwait, Uchina, Comoro pamoja na Kanada.

Novemba 2022 mauzo ya nyama ya Tanzania nje ya nchi yaliongezeka zaidi ya mara mbili hadi tani 1,423, ikiwa ni ongezeko la asilimia 125 kutoka tani 632 zilizouzwa nje ya nchi mwezi Oktoba, kwa mujibu wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB).

Nyama ya mbuzi ndiyo inayoongoza kwa mauzo ya nje ikichukua takriban asilimia 74 ya nyama inayouzwa nje ya nchi kwa tani 1,047, ikifuatiwa na kondoo (tani 343), nyama ya ng’ombe (tani 32), kuku (tani 0.67) na nguruwe (tani 0.2).

Asilimia 37 ya nyama iliyouzwa nje ya Tanzania mwezi Novemba ilikwenda Qatar, kulingana na TMB.

Thamani ya mauzo ya nyama pia iliongezeka kutoka dola 2.9 milioni (sawa na TZS bilioni 6.8) mwezi Oktoba hadi dola milioni 5.37 (TZS bilioni 12.5) mwezi Novemba.

“Kombe la Dunia liliongeza sana mahitaji ya nyama nchini Qatar, ambayo kwa sasa ni soko letu kubwa,” amesema meneja wa masoko wa TMB John Chasama .

Send this to a friend