Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali inawakaribisha wawekezaji katika sekta ya nishati ili kuongeza kasi ya usambazaji, uzalishaji na unganishwaji wa nishati nchini Tanzania.
Dkt. Biteko amesema hayo nchini Singapore wakati akishiriki mjadala kuhusu nishati akiwa pamoja na Waziri wa Madini na Nishati kutoka nchini Cambodia, Keo Rottanak na Waziri wa Maliasili kutoka nchini New Zeland, Shane Jones wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Kimataifa ya Nishati ya nchini Singapore.
“Serikali haziwezi kufanya kila kitu zenyewe hivyo ni muhimu kushirikiana na sekta binafsi. Sisi Tanzania tunawaalika sekta binafsi ije kuwekeza katika sekta ya nishati kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji, upatikanaji na usambazaji nishati na kuboresha maisha ya watu kwa ujumla,” amesema Dkt. Biteko.
Akizungunzia, ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini amesema kuwa ni matokeo ya utafiti uliofanywa na kubaini kuwa idadi kubwa ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia hali inayosababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji na uharibifu wa mazingira.
Ili kupunguza athari hizo, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeandaa mkakati unaolenga kuhakikisha Watanzania asilimia 80 wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.