Tanzania yaweka rekodi ya dunia ikiifunga Madagascar
Tanzania kuibuka na ushindi wa magoli 3-2 dhidi ya Madagascar jana pengine sio habari mpya masikioni mwako, lakini ambacho hujui ni kwamba huenda Tanzania iliweka rekodi ya dunia katika mchezo huo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.
Rekodi hiyo ni kupata penati ya mapema zaidi ambapo penati ilitolewa sekunde ya 5 baada ya mchezo kuanza kufuatia Simon Msuva kufanyiwa madhambi na mlinda mlango wa Madagascar, Melvin Adrien.
Hata hivyo, kumekuwa na mkanganyiko wa taarifa rasmi kuhusu penati ya mapema zaidi kuwahi kutolewa kwenye mpira wa miguu, lakini kabla ya mchezo wa jana, ilikuwa inaaminika kuwa penati ya Montenegro waliyopewa sekunde ya 10 baada ya mchezo wao dhidi ya Ghana kuanza mwaka 2014 ilikuwa ndiyo ya mapema zaidi.
Kufuatia ushindi wa jana, Tanzania imepanda hadi nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Kundi J ikiwa na alama 4 baada ya michezo miwili. Mchezo wa kwanza ilitoka sare (1-1) na DR Congo.