Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeondoa zuio la kutoingia nchini ililokuwa imeweka dhidi ya ndege za Shirika la Ndege la Kenya (KQ) pamoja na makampuni mengine ya nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari imeeleza kuwa mbali na KQ, zuio hilo limeondolewa pia kwa Fly 540 Limited, Safarilink Aviation na AirKenya Express Limited.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu Kenya ilipoijumuisha Tanzania katika orodha ya nchi 147 ambazo raia wake au wageni kutoka katika nchi hizo hawatotakiwa kukaa karantini kwa siku 14 kuthibitisha kuwa hawana maambukizi ya virusi vya corona (COVID19).
TCAA imesema kuondolewa kwa zuio hilo kunaanza mara moja na tayari Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Kenya imejulishwa.
Nchi hizo mbili zimekuwa na mvutano wa mara kwa mara kuhusu usafiri na usafirishaji katika mchakato wa kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo.