TAWA: Mtalii aliyewinda mamba alikuwa na kibali halali

0
32

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema uchunguzi uliofanyika umebaini mtalii aliyewinda mamba katika kitalu cha Lake Rukwa GR alikuwa na kibali halali kilichoanza Agosti 12 hadi Septemba 9, 2023.

Taarifa iliyotolewa na TAWA imesema kumbukumbu zinaonesha kuwa uwindaji huo ulisimamiwa na askari kutoka TAWA, na mwindaji bingwa kutoka kwenye kampuni iliyopewa kibali kwa mujibu wa sheria.

“Ada za tozo zote zinazohusiana na uwindaji wa mamba zililipwa kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia uwindaji hapa nchini,” imeeleza.

Imeongeza kuwa, “wakati uwindaji ukifanyika askari anayesimamia uwindaji uhakikisha uwindaji unafanyika kwa kuzingatia sheria na kulinda usalama wa wageni, wawindaji na watu walioambatana nao, hivyo taratibu zote za kisheria zilizingatiwa na hakuna utaratibu uliokiukwa.”

Aidha, TAWA imeeleza kuwa mamba huyo alikuwa na urefu wa futi 16.2 sawa na sentimita 493.8 ikiwa ni juu ya kiwango cha chini cha urefu wa sentimita 300 unaokubalika kwa mujibu wa sheria, hivyo kwa mujibu wa takwimu za taasisi za Marekani, mamba mrefu zaidi duniani aliwindwa nchini Ethiopia mwaka 2005 (futi 18.7 sawa na sentimita 561).

Send this to a friend