Tazania yatenga bilioni 4 kujenga makao makuu ya Mahakama ya Afrika

0
46

Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Imani Aboud ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kupitisha bajeti ya TZS bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za kudumu ya mahakama hiyo jijini Arusha.

”Hii ni hatua ya kihistoria na tunatarajia ujenzi wake wa haraka,” amesema na kuongeza kuwa huo ni udhihirisho mwingine wa dhamira ya Tanzania katika kupigania haki za binadamu, na watu kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), mpango wa ujenzi wa mahakama hiyo jijini Arusha ulipitishwa miaka kadhaa iliyopita, lakini haukutekelezwa.

Mtandao huo umesema unaamini kutengwa kwa fedha hizo ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinaheshimiwa na kukuzwa katika Taifa na ukanda wa Afrika.

Pamoja na pongezi hizo, wameishauri Serikali kuruhusu watu binafsi na Asasi zisizo za Kiserikali ziweze kufungua kesi moja kwa moja katika mahakama hiyo.

Mwaka 2019 serikali ilizuia watu binafsi na Asasi zisizo za Kiserikali kufungua kesi moja kwa moja kwenye mahakama hiyo ambayo kwa sasa inafanya kazi katika ofisi za muda zilizopo katika majengo ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Send this to a friend