TBA wakataa kuzungumzia suala la nyumba za Magomeni Kota

0
14

Inadaiwa Kaya 644 za Magomeni Kota zimegoma kutia saini mkataba wa kuanza kununua nyumba hizo kuanzia Februari 8, mwaka huu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuongezeka kwa bei ambayo siyo rafiki kwao.

Wakazi hao wamedai bei ya Serikali ya kati ya shilingi milioni 48 na shilingi milioni 56 haiendani na hali ya uchumi uliopo na maisha waliyonayo kwa sasa.

Taarifa iliyosomwa na Mwanasheria wa wakazi hao, Twaha Taslima iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Daud Kandoro imeeleza kua bei iliyopendekezwa na Serikali Juni mwaka jana ya TZS milioni 12 hadi TZS milioni 17 haikukidhi thamani ya eneo pia haikujumuisha faida wala huduma za maeneo yanayozunguka makazi hayo ambayo ni jumuishi.

Akizungumza Mwenyekiti wa wakazi wa Magomeni Kota, George Abel amedai bei siyo rafiki kwa wakazi hao licha ya kuongezewa kwa muda wa malipo na kuishi kutoka miaka 10 hadi 15, hivyo itawapasa kulipia TZS 300,000 kwa mwezi na TZS milioni 3.6 kwa mwaka.

“Tumepokea barua hii ikiwa zimebaki siku mbili tu kwamba tusaini mkataba wa ununuzi, tukutane tujadiliane kabla ya Februari 8 mwaka huu. Hizi bei sio rafiki, haziendani na hali za wakazi walio wengi,” amesema.

Swahili Times tulipowatafuta Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhusu sakata hilo linaloendelea hawakutoa ushirikiano wakidai tukawahoji wananchi wa Magomeni Kota.

“Wafuatane wakazi wa Magomeni Kota muwahoji kabla ya kuja kwetu,” amesema mtumishi wa TBA katika mahojiano kwa njia ya simu, licha ya kumweleza kuwa tayari tuna taarifa za upande wa wakazi hao.

Ujenzi wa nyumba hizo ulianza mwaka 2016, na wananchi alianza kuhamia mwanzoni mwaka mwaka 2022.

Send this to a friend