TBL yaadhimisha siku ya Wakulima, kuboresha mnyororo wa thamani

0
40

KAMPUNI ya Bia ya Tanzania Breweries Limited (TBL) imewahakikishia wakulima wa shayiri kuwapa ujuzi utakaowawezesha kufanya kilimo cha Kisasa na uhakika wa soko.

Mtaalamu wa Kilimo kutola TBL, Joel Msechu ameyasema hayo Jana Julai 15, 2022 wakati wa maadhimisho ya siku ya wakulima wa Shayiri mwaka 2022 yaliyofanyika Kitaifa Monduli Juu ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe.

 

Mtaalamu wa Kilimo kutoka Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Joel Msechu (mwenye miwani) akikagua mashamba ya mfano ya Zao la Shayiri, wakati wa maadhimisho ya siku ya wakulima wa shayiri yaliyoandaliwa na TBL na kufanyika kata ya Monduli Juu, Wilayani Monduli, Mkoani Arusha.

“Siku ya wakulima ya mwaka huu inayobeba kauli mbiu ya “Kilimo cha kisasa, kuboresha mnyororo wa thamani,” imeangukia msimu wa mavuno wa Shayiri, moja ya mazao muhimu ambayo TBL inanunua kwa wakulima.”

Msechu amesema wamekuwa wakiandaa maadhimisho hayo ya wakulima kila mwaka kwa miaka mingi sasa, ambapo wanatoa nafasi kwa wakulima wa shayiri na mtama kujumuika nao na kuwapa ujuzi na kutatua changamoto wanazozipitia mashambani.

Ameongeza kusema kuwa, TBL imejidhatiti kuwawezesha wakulima kwa kuwapatia masoko ya uhakika ya mazao yao na kuwapatia ujuzi utaowawezesha kufanya kilimo cha kisasa na endelevu kitakachowawezesha kukua zaidi na hatimaye kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kwenye uchumi wa taifa kama ilivyoidhinishwa kwenye kampeni ya kilimo ya Ajenda 10/30 ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kuwawezesha wakulima wadogo ni moja ya ahadi za AB InBev kama sehemu ya kutimiza malengo endelevu mwaka 2025, ambayo yanaafikiana na malengo endelevu mwaka 2025 ya umoja wa mataifa (SDG), “ amesema Msechu.

Baadhi ya wakulima wa shayiri wilaya wa Monduli Juu, wakiangalia mbegu za shayiri wakati wa maadhimisho ya siku ya wakulima wa shayiri yaliyoandaliwa na kampuni ya bia ya TBL na kufanyika wilaya ya Monduli, Arusha

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wakulima wa shayiri, wawakilishi wa TBL, mashirika ya kifedha, makampuni ya bima, maafisa ugavi na wanasayansi walioshirikishwa kwenye kuunda mbinu za kilimo na mbegu mpya.

Miaka ya nyuma, maadhimisho ya TBL ya siku ya wakulima yamedhihirisha kutoa nafasi kubwa ya kushirikishana ujuzi wa kilimo ili kukuza uzalishaji wenye tija, na vile vile kuwapa wakulima nafasi ya kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo. Vilevile, wakulima wanapatiwa mrejesho juu ya msimu ulipita na kupata nafasi ya kujifunza njia fanisi za kilimo kupitia mashamba ya mfano.

TBL hutumia nafasi hii kuonyesha utayari wake wa kufanya kazi moja kwa moja na wakulima wadogo na kuwapatia masoko ya uhakika ya mazao yao.

Mwaka jana, maadhimisho ya siku ya wakulima yalijikita kwa wakulima wa zabibu na kuainisha mafanikio makubwa kwa wakulima wa zabibu na kuingizwa rasmi kwenye kilimo cha kimkataba na TBL kwa lengo la kukuza kilimo cha zao la zabibu ili kuchangia uzalishaji endelevu wa zabibu nchini.

Send this to a friend