TBS yamtaka Masoud Kipanya kupeleka gari lake likaguliwe

0
58

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limemtaka Mtanzania mbunifu Masoud Kipanya kufika katika ofisi za shirika hilo na gari la kutumia umeme alilolibuni hivi karibuni ili liweze kukaguliwa na baadaye aweze kupata leseni na cheti cha ubora wa viwango.

Wito huo umetolewa Aprili 14, 2022 jijini Dar es Salaam na Meneja wa Viwango TBS, Yona Afrika wakati walipotembelea karakana ya mbunifu Masoud Kipanya SIDO ili kuona ubunifu alioufanya kwa kutengeneza gari la kutumia umeme.

Yona amesema wameangalia kwenye maktaba ya kitaifa wakajihakikishia viwango vya upimaji wa magari ya umeme vipo na ndivyo ambavyo watavitumia kukagua gari hilo la kisasa ili kuona hatua ya mwisho ya kupewa leseni ya ubora wa gari linalotumia umeme Tanzania inatoka.

“Lengo hasa ni kutaka kuangalia hili gari linakidhi viwango, kwa hiyo hatua ya kwanza ambayo tutaifanya kwa sababu mpaka tunakuja hapa tuliwasiliana na Masoud Kipanya pindi tu alipotangaza na kutusisitizia ngoja kwanza amalizie matengenezo ili itakapofika kipindi atakapotaka leseni ndo tweje tujiridhishe,” amesema Yona.

Kwa upande wake mbunifu wa gari hilo Masoud Kipanya ameipongeza TBS kwa kazi wanayoifanya na kwamba atayafanyia kazi yale yote ambayo ameelekezwa ili kuweza kutimiza malengo yake.

Aidha Masoud Kipanya amewashauri wabunifu wengine waliopo mitaani waweze kujitokeza na kufika TBS ili waweze kukaguliwa bidhaa zao ambazo wamebuni na kuweza kutimiza malengo yao.

Send this to a friend