TCAA yafafanua kuhusu kibali cha Helikopta ya CHADEMA

0
23

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema katika siku za hivi karibuni, hakuna chama chochote cha siasa ambacho kimeomba kibali cha kuingiza ndege nchini.

Katika taarifa iliyotolewa na TCAA kwa vyombo vya habari Oktoba 31, 2023 imesema imesikitishwa na taarifa zinazochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuhusu mamlaka hiyo kutotoa kibali kwa ndege aina ya helikopta iliyokodiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

TCAA imesema Oktoba 20 mwaka huu ilipokea ombi kutoka kwa wakala wa vibali vya ndege kwa ajili ya kuainisha maeneo ambayo viongozi wa CHADEMA watakuwa wakiruka na kutua katika maeneo yasiyo rasmi kwa lengo la kufanya mikutano ya hadhara.

“Wakala huo alishauriwa kuwasilisha ombi la kibali cha kuingiza ndege nchini kupitia mfumo rasmi ili wataalamu wetu waweze kufanya ukaguzi wa nyaraka na pia kujiridhisha na hali ya maeneo ambayo ndege hiyo ilitarajiwa kutua na kuruka kwa ajili ya usalama wa ndege, watumiaji wake pamoja na wananchi […] Wakala huo hajawahi kurudi kwetu tena kwa maombi rasmi kama alivyoelekezwa mpaka siku hii ya leo,” imeeleza taarifa.

Tanzania yashika nafasi ya 4 kwenye usalama wa anga

Imeongeza, “Kwa namna yoyote ile, mamlaka haina sababu ya kukataa kibali cha ndege ikiwa ombi na nyaraka zinakidhi vigezo. Ndege zote zilizosajiliwa nje ya nchi ni lazima ziwasilishe maombi ya kibali cha kuingia na kufanya shughuli zao nchini kupitia mfumo wa vibali kwa mujibu wa sheria. ”

Aidha, TCAA imesema CHADEMA kupitia kwa wakala wake ama kwa mmiliki wa ndege anaweza kuomba kibali cha kuingiza ndege nchini, kutua na kuruka katika maeneo yanayoruhusiwa, na kwamba ikiwa italazimu kutua katika maeneo mengine yasiyo rasmi, mamlaka hiyo kwa kutumia sheria ya Usafiri wa Anga itachambua ombi hilo na kutoa idhini iwapo vigezo vitatimia.