TCRA: Ujenzi wa kiwanda cha simu nchini kuanza 2021

0
44

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza simu nchini unaotarajiwa kuanza mwakani utaweza kurahisisha upatikanaji wa ajira kwa wahitimu kwa ngazi ya ufundi stadi nchini.

Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji wa TCRA, John Daffa amesema hayo wakati wa mahafali ya 9 ya Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasilino (TEHAMA) VETA, kilichopo Kipawa jijini Dar es salaam ambapo zaidi ya wanafunzi 200 wamehitimu kutoka kwenye Taaluma mbalimbali yenye mchepuo wa TEHAMA.

“Ujenzi wa kiwanda hicho unatazamiwa kuanza mwakani ikiwa lengo ni kusaidia kuongeza ajira na kuchochea maendeleo ya nchi ambayo ajenda yake ikiwa ni ya viwanda huku wanufaika wakuu wakiwa ni wahitimu kutoka VETA”.

Aidha amesema TCRA ina mpango wa kuondoa mafundi vishoka wa kutengeneza simu kwani wameshaanza kutoa leseni kwa wategenezaji wa simu nchini kwa ambao wamekidhi vigezo kutoka vyuo husika ambavyo ni VETA na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha VETA-Kipawa, Mhandisi Sospeter Mkasanga, amesema kuwa ujio wa kiwanda cha kutengeneza simu kwao utaongeza wigo mkubwa wa kutoa elimu huku akidai kuongeza idadi ya wanafunzi kwa mwaka ujao wa masomo.

Awali wakisoma risala wahitimu wa chuo hicho wameiomba TCRA kuwasidia kuwatatulia baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo hicho ikiwemo mabadiliko ya mitaala kuendana na kasi ya sayansi na teknolojia, muendelezo wa programu ndefu, upungufu wa vitabu kwenye maktaba ya chuo, ukosefu wa vimbweta na kukosekana kwa maeneo ya kufanya vitendo.

Nelson Rutter akiongea kwa niaba ya wazazi amewataka wahitimu kuwa na nidhamu kazini ama kwa wateja wao ili kuweza kuunda uwaminifu kwani baadhi ya mafundi wamekuwa si waaminfu kwa wateja wao.

Chuo cha TEHAMA cha VETA-Kipawa ni moja kati ya vyuo vilivyopo nchini vinavyomilikiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ambacho ni chuo cha mfano kinachotoa mafunzo mbalimbali yenye mchepuo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Send this to a friend