TCRA yaagizwa kuchunguza wizi na gharama za vifurushi vya mitandao ya simu

0
49

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amelitaka Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) kushughulikia malalamiko ya wananchi na changamoto wanazozipata wakati wanatumia huduma na bidhaa za mawasiliano nchini.

Amesema kuwa wananchi wana malalamiko kuhusu huduma wanazozipata hususani kwenye mitandao ya simu kuhusiana na mabando yao kuisha, kubadilishiwa gharama za matumizi ya mabando, kupunjwa mabando yao na fedha wanazotuma kwa njia ya mtandao na haya yote yanahitaji majibu na kupatiwa matibabu

“Hatutaki kufanya kazi kwa mazoea, nitawapima kwa matokeo na sio michakato, tutakwenda kwa mwendo wa takwimu na kila baada ya miezi mitatu tupate taarifa ya malalamiko mangapi yamepokelewa, mangapi yamefanyiwa kazi, mangapi yameisha na kwa nini mengine hayajaisha kwa kuwa haya ni mambo ya msingi ambayo tunatakiwa tuyaangalie na tuwe taasisi ya kutatua changamoto za wananchi,” amesisitiza Dkt. Ndugulile

Ameongeza kuwa ni vyema waweke mifumo ya kulinda watumiaji na walaji wa huduma za mawasiliano na bidhaa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na taarifa na siri zao kwa kuwa sekta hii inaendelea kukua na watu wanatumia biashara mtandao na hawaendi madukani.

Pia amewataka kutumia lugha nyepesi kuelimisha wananchi namna ya kutumia huduma na bidhaa za TEHAMA na wawe na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa baraza ili kutekeleza sheria ya TCRA iliyounda baraza.

Send this to a friend