TCRA yakifungia kipindi cha Shule ya Uongozi cha Humphrey Polepole
Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekisimamisha kwa muda kipindi cha Shule ya Uongozi kinachorushwa na Humphrey Polepole Online Television kutokana na kukiuka misingi, sheria na kanuni za huduma ya utangazaji.
Uamuzi huo umetengazwa na kamati hiyo mkoani Dar es Salaam baada ya kumhoji Mbunge Humphrey Polepole ambaye ndiye mmiliki wa televisheni hiyo na mwendeshaji wa kipindi husika kinachoruka kupitia mitandao ya kijamii.
Kamati imetoa masharti ya kipindi hicho kufunguliwa ambapo, sharti la kwanza ni kituo hicho kuwa na watumishi wenye taaluma ya uandishi na utangazaji wa habari ili kuleta tija katika vipindi vyake. Awali kamati imeeleza kwamba televisheni hiyo haina watumishi wenye taaluma husika hivyo kupelekea kukiuka sheria, misingi na kanuni za taaluma husika.
Pili, kuhakikisha vipindi vyake vyote vinazingatia sheria, kanuni, na misingi ya uandishi na utangazaji wa habari pamoja na masharti ya leseni yake.
Baada ya kutimiza masharti hayo, kituo hicho kitatoa taarifa TCRA, ambapo ikijiridhisha kuwa maelekezo yote yamezingatiwa, kipindi cha Shule ya Uongozi kitarejea na kuwa chini ya uangalizi wa mamlaka hiyo kwa miezi sita.
Kituo hicho pia kimepewa onyo kali baada ya kuthibitika kuwa maudhui ya kipindi ni ya upotoshaji na yanayoweza kusababisha taharuki kwa wananchi.
Katika vipindi tofauti Polepole amekutwa na hatia kwa kusema kuwa virusi vya UVIKO19 vimetengenezwa na kampuni kubwa ili kuuza chanjo na kujipatia fedha, madai ambayo hakuweza kuthibitisha na hakutoa nafasi kwa mtaalamu wa afya kutoa ufafanuzi. Kamati imeeleza zaidi kuwa madai haya yanadhoofisha jitihada za mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Pia, amekutwa na hatia ya kusema kuwa deni la Taifa limekuwa kubwa sana, na kuwataka viongozi kutoa ufafanuzi, lakini hakuwa na kiongozi kwenye kipindi kutoa ufafanuzi huo. Aidha, kamati imethibitisha kuwa waziri wa fedha alitoa ufafanuzi bungeni kuhusu deni na kusema kwamba ni himilivu.