TCRA yasitisha kwa muda leseni ya utoaji maudhui mtandaoni ya Mwananchi Newspaper

0
36

Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) kupitia Kamati yake ya Maudhui imesitisha leseni ya utoaji huduma za maudhui mtandaoni ya Mwananchi Newspaper kwa muda wa miezi sita. Tovuti ya gazeti hilo, (mwananchi.co.tz) ni moja ya tovuti za habari zinazotembelewa kwa wingi zaidi nchini Tanzania, kwa mujibu wa takwimu za mitandao ya Alexa na SimilarWeb. 

Sambamba na kusimamishwa huko, gazeti hilo limetakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 5 za Kitanzania kwa kosa la kukiuka Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui Mitandaoni) 2018. 

Taarifa ya TCRA ya Aprili 16 imeeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika kuwa Aprili 13 2020, kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za gazeti hilo (Mwananchi Newspaper) lilichapisha na kutangaza taarifa yenye kupotosha na kuleta mkanganyiko kwa jamii, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. 

TCRA imeongeza kuwa, baada ya tukio hilo, kwa mujibu wa kanuni, Mwananchi Newspaper waliitwa mbele ya Kamati ya Maudhui Aprili 15 2020 kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kosa hilo ambalo walikiri kulitenda. Baada ya maelezo, TCRA ilijiridhisha kuwa kosa hilo lilitendeka na kutoa adhabu hiyo.

Send this to a friend