TCRA yatolea ufafanuzi sheria ya umiliki wa laini moja iliyoanza kutumika leo

0
12

Sheria ya umiliki wa laini moja ya simu kwa kila mtandao imeanza kutumika leo Julai Mosi 2020 ambapo ndio siku ya kwanza ya mwaka wa fedha wa serikali.

Hata hivyo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuwa sheria hiyo haimzuii mtu kumiliki laini zaidi ya moja kwa mtandao mmoja, isipokuwa atalazimika kutolea ufafanuzi laini ya ziada, na kwamba lengo la sheria hiyo ni kudhibiti umiliki holela wa laini za simu na kudhibiti uhalifu.

“Kuna wengine wanasajili [laini zaidi ya moja] kwa ajili ya matumizi ya biashara au majumbani, hivyo huwezi kuwafunga kwa kuwaambia wamiliki laini moja,” amenukuliwa Msemaji wa TCRA, Semu Mwakyanjala wakati akizungumza na Gazeti la Mwananchi.

Kifungu cha 18 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, sheria ya usajili wa laini za simu ya mwaka 2020 inaeleza kuwa mtu anatakiwa kumiliki laini moja ya simu kwa mtandao kwa ajili ya matumizi ya kupiga, kutuma jumbe na huduma za intaneti.

Sheria hiyo inaeleza kuwa mtu atakayemiliki laini zaidi ya moja kwa mtandao kinyume cha sheria atatozwa faini ya TZS 5 milioni au kifungo jela kwa miezi 12 au vyote kwa pamoja.

Na katika kila siku ambayo laini ya ziada ilitumika mhusika atalipa faini ya TZS 75,000 kwa siku.

Aidha, sheria hairuhusu kampuni kumiliki laini zaidi ya 30 ambazo zitatumika katika kupiga, kutuma jumba au huduma ya intaneti. Endapo kampuni itakiuka sheria hiyo, itatozwa faini isiyopungua TZS 50 milioni pamoja na TZS 175,000 kwa kila siku ambayo laini za/ya ziada ilitumika.

Unaweza kuangalia idadi ya laini za simu zilizosajiliwa kwa jina lako kwa kupiga *106# ambapo ukichagua namba mbili utapata idadi ya laini zilizosajiliwa kwa jina lako katika mtandao husika, na ukichagua namba 3 utaona idadi ya zilizosajiliwa kwa jina lako katika mitandao yote.

Wananchi kupitia mitandao ya kijamii wameonekana kuilalamikia sheria hiyo ambayo baadhi wamedai kuwa inaminya uhuru wao.