TCRA yavichukulia hatua vituo 8 vya habari kwa kukiuka sheria

0
44

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kupitia Kamati ya Maudhui imevichukulia hatua mbalimbali vituo tisa vya habari kwa kukiuka sheria na kanuni za utangazaji kwa kurusha maudhui bila kuzingatia mizania ya habari na kurusha maudhui yasiyostahili.

Akitoa maelezea hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Joseph Mapunda ametaja vituo vilivyochukuliwa hatua kuwa ni pamoja na Radio Free Africa, Radio One Stereo, CG FM na Abood FM.

Vituo hivyo vitatu vimechukuliwa hatua kwa kurusha maudhui yasiyozingatia mizani kupitia kipindi cha Amka na BBC ambapo Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu aliishutumi serikali kuwazuia viongozi wa chama hicho kuuaga mwili wa Hayati Benjamin Mkapa.

Mapunda amesema kuwa vyombp hivyo vilirusha taarifa hiyo bila kutafuta ufafanuzi kutoka kwa Msemaji Mkuu wa Serikali na vimewekwa chini ya uangalizi kwa muda wa miezi mitatu (CG FM na Abood FM miezi sita) kuhakikisha havirudii kosa hilo.

Mbali na vituo hivyo, TCRA imekifungia kipindi cha Jahazi kinachorushwa na Clouds FM kwa kosa la kurusha maudhui yanayochochea kujichua sehemu za siri, kosa ambalo kamati imesema limekuwa likijirudia. Kamati imesema kituo hicho kisijaze muda huo kwa kipindi kingine chenye maudhui kama jahazi.

Kituo cha Wasafi Media Online TV kimetozwa faini ya TZS 5 milioni kwa kurusha maudhui yanayochochea ngono kupitia kipindi cha Women Matters. Aidha, kituo hicho pia kilirushwa taarifa za kuwakebehi baadhi ya wagombea waliochukua fomu huku kikiwapigia kampeni wengine.

Hata hivyo shtaka la kukebehi na kuwapigia kampeni wagombea wa uchaguzi limetupiliwa mbali kw akukosekana ushahidi usio na shaka.

Kwa upande mwingine kituo cha televisheni ya mtandaoni cha Carry Mastory kimetozwa faini ya TZS 5 milioni kwa kurudha maudhui yaliyoegemea upande mmoja, kutumia lugha isiyo na staha za uandishi na kurusha maudhui yanayochochea ngono kinyume na maumbile.

Wakati huo huo, CG FM imeonya na kuwekwa chini ya uangalizi na kupewa onyo kali kwa kosa la kukiuka agizo la serikali lililotolewa mwaka 2017 la kuzuia vyombo vya habari kusoma kwa kina habari zilizomo kwenye magazeti, badala yake wasome vichwa vya habari tu.

Kituo cha redio cha Triple A FM cha jijini Arusha kimetozwa faini ya TZS 5 milioni, kimewekwa chini ya uangalizi kwa miezi mitatu na kupewa onyo kali kwa kosa la kurusha maudhui yanayochochea ushirikina.

Wakati huo huo, Kamati hiyo imetupilia mbali shutuma zilizotolewa dhidi ya kituo cha redio cha Kiss FM kuhusu kurusha maudhuI Amka na BBC yasiyozingatia mizani ya habari. Shutuma hiyo imetupiliwa mbali kwa sababu redio tajwa haina kipindi cha Amka na BBC.

Send this to a friend