Teknolojia inavyosaidia wanafunzi kuendelea na masomo

0
31

Jana, Juni Mosi wanafunzi wa vyuo pamoja na kidato cha sita kote nchini wamerejea shule baada ya shule na vyuo kufungwa kwa takribani miezi miwili na nusu na Serikali kama moja ya hatua za mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Korona nchini. Kwa vyovyote mazingira ya kusoma kwa wanafunzi hawa yamebadilishwa na namna sote kama jamii tunavyoshiriki mapambano haya dhidi ya Korona haswa haswa kwa kufuata ushauri wa wataalam wa afya.

Mabadiliko haya ya mazingira na namna ya utoaji na upokeaji elimu yalianza pale shule na vyuo zilipofungwa rasmi mwezi Machi. Iliwalazimu wanafunzi, walimu, wazazi na walezi kuja na mbinu mbadala za kuyageuza mazingira ya nyumbani kuwa mazingira rasmi ya utoaji na upokeaji mafunzo.

Hapa tumeona namna teknolojia ilivyochangia kwa kiasi kikubwa kusaidia kutatua changamoto ya wakufunzi na wanafunzi kutokuwepo katika eneo moja. Tumeshuhudia mitandao maarufu duniani kama vile YouTube, Khan Academy na kadhalika iliyosheheni mihadhara toka kwa wakufunzi wa masomo mbalimbali duniani ikitumika zaidi na zaidi kipindi hiki katika elimu. Teknolojia nyingine kama Zoom, Skype na kadhalika zimetumika na wakufunzi kuendelea kufundisha wanafunzi wakiwa mbali na shule. 

Pia tumeshuhudia ubunifu wa wazawa hapa hapa Tanzania ukichangia katika ufumbuzi wa utoaji elimu katika mazingira haya. Ubunifu huu ni kama instantschools ya Vodacom Tanzania, smartclass, shuledirect, mtabeapp pamoja na jitihada za watu/wakufunzi/walimu binafsi au shule kupitia mitandao ya kijamii kama whatsapp, facebook, instagram na twitter. Mwanafunzi na mkufunzi wakiwa na simu janja na bando (intaneti) basi wanakuwa na uwezo wa kutumia njia hizi mbalimbali za kutoa ama kujipatia mafunzo/elimu. Jitihada zote hizi zinachangia, kwa sehemu, katika kufumbua changamoto ya mazingira ya elimu pale ambapo walimu na wanafunzi hawajaweza kuwa katika eneo moja. 

Katika kuchangia tena kwenye ufumbuzi wa changamoto hii tumeona makampuni kama Vodacom Tanzania wamewezesha wateja wao kuperuzi baadhi ya tovuti zenye maudhui muhimu katika elimu na upatikanaji taarifa muhimu kuhusu Korona toka serikalini bila kuhitaji bando. Yaani hata ukiwa na MB sifuri! Hisham Hendi, CEO wa Vodacom Tanzania ameeleza kuwa Vodacom Tanzania kama sehemu ya jamii ya Tanzania waliona umuhimu wa kuwawezesha wanafunzi wa ngazi mbali mbali za masomo kuperuzi bure baadhi ya tovuti zenye maudhui ya elimu katika kipindi ambacho shule zimefungwa kutokana na Korona. Tovuti hizo ni Vodacom Instant Schools, Smart Class, DIT E-learning, Smart Class Africa, UDSM Learning Management System na Shule Direct. Tovuti nyingine muhimu zinazopatikana kwa wateja wa Vodacom Tanzania hata wakiwa na MB sifuri ni tovuti ya Wizara ya Afya, Wizara ya Habari pamoja na Habari Maelezo.

Wanafunzi wa vyuo na kidato cha sita wanarudi shule na kuendelea ma masomo huku mashule na vyuo vikifuata miongozo mbali mbali iliyotolewa na serikali pamoja na wataalam wa afya ili kuhakikisha usalama na afya za wanafunzi, wakufunzi na jamii kwa ujumla. Mambo kama kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kuhakikisha umbali wa walau mita moja mpaka mbili kati ya mtu na mtu kwavyovyote sasa ni sehemu ya utoaji na upokeaji mafunzo/elimu mashuleni na vyuoni. Hii pia ni sehemu muhimu ya ufumbuzi wa changamoto za mazingira ya elimu katika kipindi cha janga la Korona. 

Teknolojia itaendelea kutumika sana kwenye mazingira ya elimu katika maeneo mbali mbali mfano usajili, mikopo ya elimu ya juu, malipo, mihadhara, mijadala, warsha, majaribio, mitihani, tafiti, shughuli za maktaba, mawasiliano n.k. Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia baraza la Baraza la Ushauri wa Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA-CCC) umeziandikia barua kampuni za mawasiliano ya simu kupunguza gharama za intaneti. Hii pia itachangia kwenye ufumbuzi wa changamoto ya mazingira ya elimu katika kipindi hiki. 

CEO wa Vodacom Tanzania Bw. Hisham Hendi ametoa rai kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya umma kuwasilisha tovuti zao Vodacom kupitia  www.vodacom.co.tz ili wanafunzi waweze kuziperuzi bure – hata wakiwa na MB sifuri. Huu ni mwendelezo mzuri wa ufumbuzi wa changamoto za mazingira ya elimu katika kipindi hiki. Makampuni mengine ya simu nchini nayo yakifanya hivi hakika itakuwa mchango mkubwa sana kwa wanafunzi na walimu/wakufunzi.

Hakuna ufumbuzi mmoja pekee unaojibu changamoto zote za elimu katika kipindi hiki cha janga la korona. Kuna changamoto ambazo bado zipo na zinahitaji ufumbuzi bado kwa mazingira ya elimu kwa wanafunzi/wakufunzi wenye ulemavu na wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wakufunzi wao. Kuna wanafunzi/wakufunzi ambao ambao hawana simu janja, kompyuta, umeme, mtandao, bando nk.  Itachukua jitihada za wadau wote wa elimu – sekta binafsi na ya umma, wakufunzi, wanafunzi, wazazi, walezi na jamii yote kwa ujumla – kuwa wabunifu na kuchangia kwa namna tunayoweza. Kwa umoja wetu tutafumbua zaidi na zaidi changamoto hizi.

Send this to a friend