Zaidi ya watu 500 wamefariki na wengine takribani 2,000 kujeruhiwa baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa magnitudi 7.8 kupiga eneo la kusini mwa Uturuki karibu na mpaka wa Syria mapema Jumatatu Februari 06, 2023.
Tetemeko hilo ambalo limedaiwa kuwa ni moja ya tetemeko lenye nguvu zaidi kuwahi kutokea katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 100, limepiga kilomita 23 mashariki mwa Nurdagi mkoa wa Gaziantep kwa kilomita 24.1 (maili 14.9).
Shirika la Maafa la Uturuki limeomba msaada kutoka Jumuiya ya Kimataifa katika shughuli za uokoaji huku maofisa wa Uturuki na Syria wakieleza kuwa idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka.
Waokoaji wanaendelea kuokoa watu waliokwama chini ya vifusi baada ya mamia ya majengo kuporomoka katika nchi zote mbili, huku Uturuki ikitangaza hali ya hatari na kuwataka watu kutotumia simu za rununu (mobile phone) ili kuruhusu waokoaji kufanya uokoaji.
Aidha, Rais wa Marekani, Joe Biden ameagiza Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) pamoja na washirika wa Serikali kuu kutathmini njia za kukabiliana na walioathiriwa zaidi na tetemeko hilo akiahidi kuwa Marekani iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika.