Mmoja wa wasimamizi wakuu wa bima na mali duniani, The Allianz rasmi sasa wamekuwa wanahisa wakubwa zaidi wa Jubilee General Insurance Company of Tanzania Limited.
Muamala uliofanyika unaonesha kuwa Allianz itakuwa na hisa asilimia 51 kutoka kwa Jubilee Holdings Limited na Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED), huku Kampuni ya Jubilee Holdings Limited (JHL) ikibaki na asilimia 15 ya hisa, na wanahisa wengine sita wadogo watakuwa na umiliki wa hisa asilimia 34.
Kama sehemu ya ununuzi huo, Kampuni ya Jubilee General Insurance Company of Tanzania Limited itabadilisha jina lake na kuwa Jubilee Allianz General Insurance Company Limited, hata hivyo itasubiri kuthibitishwa.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kundi la Jubilee Holdings, Nizar Juma amesema uunganaji wa Jubilee Holdings na Allianz SE, kwa mara nyingine tena zimeimarisha dhamira ya kupanua bima nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
“Uwezo wa pamoja wa chapa hizi mbili unatupa fursa nzuri ya kukuza zaidi tasnia ya bima katika soko la Tanzania. Harambee hizi zitasaidia sana kuiweka Tanzania kwenye daraja la juu zaidi katika suala la kupenya kwa bima,” amesema Juma.