TIC yasajili miradi ya trilioni 7 Julai hadi Novemba 2022

0
50

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), John Mnali amesema kituo hicho kimesajili jumla ya miradi 132 yenye thamani ya dola za Marekani 3.16 bilioni (takribani Sh7 trilioni) katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2022.

Ameyasema hayo leo Desemba 27, 2022 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amebainisha kuwa miradi hiyo ni ongezeko la asilimia 22.2 ukilinganisha na miradi 108 iliyosajiliwa mwaka 2021.

Mnali amesema kati ya miradi hiyo, 50 inamilikiwa na wawekezaji kutoka nje ya nchi, 30 ya wazawa na 52 imetokana na ubia kati ya Watanzania na wageni huku sekta ya viwanda ikiongoza kwa kusajili miradi 67 ikifuatiwa na usafirishaji yenye miradi 25 katika miradi iliyosajiliwa mwaka huu.

Sekta ya utalii imesajili miradi 12, kilimo miradi tisa, huduma mbalimbali miradi minane, majengo na biashara saba, rasilimali watu miradi mitatu na sekta ya fedha ikisajili mradi mmoja.

“Miradi hiyo inatarajiwa kutoa ajira 21,297 ambayo ni ongezeko la asilimia 57 kutoka ajira 13,578 zilizozalishwa mwezi Julai hadi Novemba mwaka jana,” amesema.

Send this to a friend