Timu ya Taifa ya Nigeria yasusia mechi ya kufuzu AFCON

0
34

Timu ya Taifa ya Nigeria imeamua kutocheza mechi ya kufuzu Mashindano ya AFCON 2025 nchini Libya dhidi ya Mediterranean Knights baada ya kukabiliwa na mazingira magumu tangu walipowasili Jumapili nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) imesema wachezaji wameamua kutocheza tena mechi hiyo baada ya kukwama uwanja wa ndege kwa zaidi ya saa 15 huku ikiilaumu Shirikisho la Soka la Libya kwa kutotuma timu yoyote ya mapokezi au hata magari ya kuwachukua wajumbe kutoka uwanja wa ndege hadi hotelini, ambapo ni takriban saa 3.

Nahodha wa timu hiyo, William Troost-Ekong amesema kuwa hawatakubali kusafiri kwa basi kwa muda wa saa tatu kutoka uwanja wa ndege wa Al-Abraq hadi Benina, ambapo mechi ya kufuzu imepangwa kufanyika Jumanne, kwa sababu za kiusalama.

“Kama nahodha wa timu, pamoja na timu, tumeamua HATUTACHEZA mechi hii. “Waacheni wapate pointi. Hatutakubali kusafiri kokote kwa barabara hapa; hata ikiwa kuna ulinzi, si salama. Tunaweza kufikiria jinsi hoteli au chakula ambavyo kingekuwa kama tungeendelea,” ameandika kwenye mitandao ya kijamii.

BASATA yalaani tukio la Zuchu kutupiwa vitu jukwaani

Aidha, mchezaji wa zamani bora wa Afrika, Victor Ikpeba, ambaye aliandamana na timu hiyo kwenda Libya, ameunga mkono uamuzi wa kususia mechi na kuitaka Libya ipigwe marufuku kushiriki michezo hiyo na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Hayo yamejiri siku chache kufuatia malalamiko ya Libya kudai kutendewa visivyo wakati walipowasili Nigeria kwa ajili ya mchezo wao huko Uyo, ambapo viongozi wa Libya walidai kuwa walirudishwa hadi Port Harcourt badala ya Uyo ambako mechi hiyo ilikuwa ikifanyika, na hivyo kuzua mvutano kati ya timu hizo.

Kwa sasa Nigeria wanaongoza Kundi D la mchujo wakiwa na pointi 7, huku Libya wakishika mkia kwa kuwa na pointi 1 pekee.