Tito Magoti na Theodory Giyan waachiwa huru baada ya kulipa milioni 17
Afisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti na mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Theodory Giyan wameachiwa huru baada ya kukubali kulipa TZS milioni 17.
Wawili hao walikamatwa Disemba 20, 2019 na walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Disemba 24, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakishitakiwa kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi likiwemo la utakatishaji fedha kiasi cha TZS milioni 17 katika kesi Na. 137 ya mwaka 2019.
Kwa muda wote huo wawili hao walikuwa rumande kutokana na makosa hayo kutokuwa na dhamana, huku kesi hiyo ikiahirishwa mara 26, kabla ya leo kuachiwa huru baada ya makubaliano ya kulipa fedha kufikiwa.
Katika kesi ya msingi, Magoti na Giyan walidaiwa kushiriki genge la uhalifu, kosa wanaodaiwa kulitenda katika tarehe tofauti kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 jijini Dar es Salaam na katika maeneo mbalimbali ya ndani ya nchi. Ilielezwa kuwa makusudi walishiriki makosa ya uhalifu ikiwa ni kumiliki programu za kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kufanya uhalifu.
Katika shtaka la pili, washitakiwa hao walidaiwa siku na eneo hilo, kumiliki programu za kompyuta kwa lengo la kutenda kosa la uhalifu.
Katika shitaka la tatu, ambalo ni kutakatisha fedha, jamhuri ilieleza kuwa Magoti na Giyan, wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ndani ya nchi.
Wanashtakiwa hao walidaiwa katika tarehe hizo, walijipatia TZS 17.35 milioni wakati wakijua fedha hizo ni zao tangulizi la kushiriki genge la uhalifu.