TLS: Tunataka ‘Afande’ afikishwe mahakamani

0
86

Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kimelitaka Jeshi la Polisi kumfikisha mahakamani mtu aliyetambulika kwa jina la ‘afande’ ambaye anadaiwa kuwatuma vijana wanne waliohusika kumbaka na kumlawiti binti kisha video hizo kusambaa mitandaoni.

Akizungumza na vyombo vya Habari, rais wa TLS, Boniface Mwabukusi amesema mtu huyo aliye nyuma ya tukio hilo amehusika kwenye uhalifu huo hivyo afikishwe mahakamani mara moja, huku akieleza kuwa TLS itafuatilia kwa ukaribu shauri hilo ili binti huyo apate haki yake.

“Tunataka aliyesababisha kitendo kile kufanyika na yeye ni mkosaji, afikishwe mahakamani mara moja. TLS itaona namna bora ya kuweka wakili atakayekuwa akifuatilia ili kuona maendeleo ya shauri lile yatakavyokuwa yakiendelea na kuhakikisha kuwa haki za binti yule hazipotei,” amesema Mwabukusi.

Aidha, TLS imelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua iliyoichukua ya kumuadabisha RPC wa Dodoma kwa kitendo alichokifanya ambacho TLS imesema kuwa kinaonesha kuunga mkono au kupuuzia uhalifu aliofanyiwa binti huyo.

Mbali na hayo, TLS imetoa wito kwa Jeshi la Polisi na Wizara yenye dhamana kuimarisha madawati ya jinsia katika jeshi la polisi ili kuweza kushughulikia changamoto ya ukatili wa kijinsia ipasavyo, na isiwe madawati kama jina.

Send this to a friend