TMA yatoa tahadhari kipindi cha vuli

0
31

Mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA) imesema kuna uwezekano wa kutokea kwa athari za uzalishaji wa mazao katika msimu wa mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba hadi Disemba, ambapo utabiri unaonesha maeneo mengi ya nchi yatapata mvua za chini ya wastani hadi wastani.

Akitoa utabiri huo leo Septemba 02, 2022 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu TMA, Dkt. Agnes Kijazi amesema upungufu wa unyevu unyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, hivyo ameshauri wakulima kupanda kwa wakati, kutumia mbegu na mazao yanayoweza kukomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame.

Kijazi amesema katika msimu huo kuna uwezekano wa kutokea kwa migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, hivyo wafugaji na wavuvi waweke mipango madhubuti ya matumizi sahihi na uhifadhi wa maji ya malisho ya mifugo.

Aidha, Mamlaka imeishauri jamii kwa ujumla kutumia chakula kwa uangalifu katika ngazi ya kaya pamoja na ngazi ya kitaifa pamoja na jamii kutegemea joto kali kuliko kawaida hasa katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.

Send this to a friend