TMA yatoa tahadhari uwepo wa kimbunga CHIDO Bahari ya Hindi

0
13

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya uwepo wa kimbunga ‘CHIDO’ katika Bahari ya Hindi, Kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.

Taarifa iliyotolewa na TMA imesema mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kinatarajiwa kuelekea maeneo ya Kaskazini mwa Msumbiji katika kipindi cha siku nne, kuanzia Desemba 13 hadi 16 mwaka huu na kwamba kwa sasa kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja nchini.

“Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga hicho kinatarajiwa kupita (Kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya Kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa itakayoambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa ya Bahari kwa maeneo ya Mtwara na maeneo ya jirani hususan kati ya tarehe 14 na 16, Desemba 2024,” imesema TMA.

Aidha, TMA imetoa tahadhari kwa watumiaji wa Bahari na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Send this to a friend