Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mgandamizo wa hewa katika Bahari ya Hindi, Mashariki mwa pwani ya Mtwara kama ilivyoelezwa katika taarifa iliyotolewa Mei 1, 2024 umeendelea kuimarika na kuwa kimbunga ‘HIDAYA’ chenye nguvu ya kati, kikiwa umbali wa takriban Kilomita 506 Mashariki mwa Pwani ya Mtwara.
Katika taarifa iliyotolewa na TMA imesema mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga HIDAYA kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania kuanzia usiku wa leo Mei 02, 2024 na kuendelea kuwepo hadi Mei 06, 2024, na kwamba kimbunga hicho kinatarajiwa kupungua nguvu baada ya Mei 6, mwaka huu.
“Uwepo wa kimbunga HIDAYA karibu na pwani ya Tanzania unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani hususan tarehe 3 Mei 2024 kwa maeneo ya pwani ya kusini (Lindi na Mtwara) na kusambaa katika maeneo mengine ya ukanda wa Pwani kuelekea Mei 4 hadi 6 2024,” imesema.
TMA imewatahadharisha wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini kuchukua tahadhari kubwa na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka TMA, pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.