Chama cha Wanasayansi wa Magonjwa ya Mishipa ya Fahamu Tanzania (TNA), kimesema asilimia 75 ya watu wenye kifafa hupelekwa kwanza kwa waganga wa kienyeji na viongozi wa kiroho badala ya hospitali hali inayopelekea ugumu wakati wa kuudhibiti.
Akizungumza mwenyekiti wa TNA, Profesa William Matuja katika Kongamano la maadhimisho ya siku ya kifafa duniani yanayofanyika Februari 12 kila mwaka duniani, amesema idadi kubwa ya watu nchini wana imani potofu kuhusu kifafa, ambapo zaidi ya asilimia 36 bado wanaamini ugonjwa wa kifafa unatokana na nguvu za giza ikiwemo mapepo wachafu.
Aidha, amefafanua kuwa asilimia 26 ya wagonjwa wa kifafa wana matatizo ya kimwili kutokana na mshtuko wa moyo ambao haujatibiwa ikiwa ni pamoja na makovu mwilini, majeraha ya moto, mikazo, kuteguka kwa viungo hasa mabega, kuumia kichwa na vifo vya mapema.
P2 inavyosababisha madhara kwenye hedhi na mifupa
“Kifafa ni ugonjwa unaotokana na hitilafu au jeraha kwenye ubongo, linalosababisha mgonjwa kuanguka, kukakamaa kuzimia au kutokuzimia na wakati mwingine kutoa povu mdomoni,” amesema Profesa Matuja.
Ameongeza kuwa zaidi ya watu milioni 60 wanaishi na kifafa duniani kote, huku bara la Afrika likiwa ndilo bara lililoathirika zaidi na tatizo hilo ambapo katika watu 1,000, watu kati ya 20-50 wanaishi na tatizo hilo.