Tofauti ya Shahada ya Udaktari wa Heshima na Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD)
Mjadala mkubwa umeibuka katika mitandao ya kijamii hasa baada ya Mbunge wa Geita Mjini, Joseph Kasheku Musukuma kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Siasa na Uongozi (Honoris Causa in Politics and Leadership) na Chuo cha Academy of Universal Global Peace cha Marekani.
Mjadala huo umeletwa na hoja kama Musukuma atatumia utambulisho wa ‘Dk.’ kabla ya jina lake ama la. Kabla ya kujibu swali hilo, ni vyema tofauti ya udaktari huo ukawekwa bayana.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Godlisten Malisa amewahi kueleza kiundani utofauti wa zote mbili. Alieleza kwamba zinatofautiana kwani Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD) inasomewa darasani, inafanyiwa utafiti, na utafiti huo unatetewa kwenye jopo la maprofesa. Lakini Shahada ya Udaktari wa Heshima inatolewa bila kusomewa kwa mtu yeyote aliyefanya jambo kubwa lililogusa jamii.
Bodi ya chuo husika hukaa na kuangalia mtu aliyefanya jambo kubwa kwa jamii wanamtunuku Shahada ya Udaktari wa Heshima kama njia ya kutambua mchango wake. Mfano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sanaa (FPA) kinaweza kumtunuku Diamond Platnumz Shahada ya Udaktari wa Heshima kama njia ya kutambua mchango wake katika kukuza sanaa kupitia muziki.
Kuna shahada za udaktari wa aina nyingi. Kwa uchache kuna Shahada ya Udaktari wa Binadamu (MD), Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD), Shahada ya Udaktari wa Sheria (LLD), Shahada ya Udaktari wa Sheria za Kanisa (JCD), Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa).
Mifano ya shahada hizo inaweza kutofautishwa kwa kuwaangalia watu hawa na shahada walizonazo. Dk. Benson Bagonza (PhD), Dk. Chris Cyrilo (MD), Dk. Wilbroad Slaa (JCD), Dk. Seng’ondo Mvungi (LLD) na Dk. Jakaya Kikwete (Honoris causa).
Hakuna sheria, kanuni au mwongozo unaomzuia mtu mwenye Shahada ya Udaktari ya Heshima kuanza na utambulisho wa ‘Dk’ kabla ya jina lake, japo baadhi hawafanyi hivyo, na wale wanaopata udaktari kwa kusoma, baadhi hawapendi kuona wanaopewa kwa heshima wakitumia utambulisho huo.
Mifano ya waliotunukiwa lakini hawatumii ni pamoja na Bill Clinton ambaye ametunukiwa mara tatu, Mwl. Julius Nyerere alitunukiwa mara 8 na vyuo mbalimbali vyenye hadhi na hivi karibuni mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima na Manchester University, moja ya vyuo vikubwa sana duniani, lakini hajiiti Dk. Rashford.
Hivyo basi, suala la kutumia utambulisho huo ama kutotumia mara nyingi ni la mhusika mwenyewe.