TPA yakanusha kuipa DP World uendeshaji wa Bandari ya Dar kwa miaka 100

0
64

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa Serikali imepanga kuipa kampuni ya DP World ya Dubai kandarasi ya uendeshaji wa shughuli za Bandari ya Dar es Salaam kwa muda wa miaka mia moja ni upotoshaji unaofanywa kwa makusudi na watu wenye nia ovu.

Katika taarifa yake, TPA imeeleza kwamba Azimio la Bunge linahusu mkataba ambao Serikali ya Tanzania inaingia na Serikali ya Dubai wenye ukomo wa miezi 12 kwa ajili ya kutoa nafasi kwa Serikali ya Tanzania kujadiliana na Serikali ya Dubai kuhusu maeneo ambayo Serikali hizo mbili zinaweza kushirikiana katika uboreshaji na uendelezaji wa sekta ya bandari nchini.

Kwanini Tanzania imechagua kuingia makubaliano na kampuni ya Dubai kuboresha Bandari ya Dar?

“Ushirikiano wa Dubai na Tanzania una lengo la kuongeza ufanisi wa huduma za bandari nchini, kukuza ajira za Watanzania na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kupitia uwekezaji kwenye baadhi ya maeneo ya Bandari ya Dar es Salaam, maeneo huru ya kiuchumi na viwanda (Special Economic and Industrial Zones) kwa kujenga viwanda na uwekezaji katika mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka Bandari ya Tanzania kwenda nchi za jirani ambazo zinatumia bandari zetu,” imesema TPA.

Aidha, TPA imeeleza kuwa jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuvutia uwekezaji nchini hususani katika maeneo ya bandari, zinalenga kumaliza changamoto za muda mrefu ikiwemo ucheleweshaji wa meli, mizigo na kukosekana kwa ufanisi.