TRA: Tozo ya kitanda nyumba za kulala wageni sio utaratibu mpya

0
16

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo amesema utaratibu wa ukusanyaji wa kodi ya kitanda katika mahoteli na sehemu zote za kulala wageni sio utaratibu mpya hivyo kinachofanyika ni utoaji wa elimu na kuwakumbusha wamiliki kujua wajibu wao na kuutekeleza.

Akizungumza na Swahili Times Januari 14, 2022 kuhusu taarifa ya wamiliki wa nyumba za wageni kulipia tozo hiyo, Kayombo amefafanua kuwa utaratibu huo ni sheria ya mwaka 2008 na kanuni za 2013 za sheria ya utalii.

Ameongeza kuwa kodi hiyo inatokana na idadi ya wageni waliolala katika hoteli husika, hivyo orodha ya vitanda vinavyojumuishwa ni kutoka katika aina zote za malazi ya wageni ikiwemo hoteli kubwa, ndogo, za kati na ‘guest house’.

“Mgeni popote ni mgeni, mtalii haimaanishi atoke Ulaya ndipo aje, hata ukitoka unapoishi ukaenda Dodoma, ukaenda Mbeya wewe ni mtalii katika ule mji, kwahiyo unapolala pale mwenye hoteli anao wajibu wa kuorodhesha wageni waliolala na kiasi kinachotakiwa kutozwa katika hayo mapato waliyoyapata,” amefafanua.

RC Sendiga apiga marufuku watumishi kuhama Mkoa wa Rukwa

Kayombo amebainisha kuwa awali kodi hiyo ilikuwa ikitozwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kisha ikahamishiwa TRA, hivyo wizara hiyo inao wajibu kila mara kuorodhesha hoteli na nyumba za kulala wageni ambapo orodha hiyo ndiyo inayotumika katika kufuatilia utozaji wa tozo.

“Hiyo kodi ipo kwa ajili ya kuendeleza utalii nchini, kwa hiyo sisi tunafanya kuikusanya kwa niaba ya Serikali kwa sababu tunayo miundombinu kwa kuwa na ofisi nchi nzima, kwa hiyo sio kitu kipya,” amesema Kayombo.

Kuwa mujibu wa sheria, tozo ya kitanda ni asilimia moja (1%) ya gharama ya chumba ambacho mtalii (mteja) analipia kulala kwenye chumba husika.

Send this to a friend