TRA: Ukamataji unafanyika tunapofanya ukaguzi kujiridhisha

0
37

Kufuatia malalamiko yanayotolewa na wafanyabiashara wa soko la Kariakoo kuhusu kamata kamata inayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mamlaka imeeleza kuwa hatua hiyo hutokea pindi wanapofanya ukaguzi ili kujiridha usahihi wa utoaji wa risiti.

Akizungumza na Swahili Times, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA, Richard Kayombo amefafanua kuwa mtu akikamatwa maana yake hajatoa risiti kwa usahihi.

“Kama mtu ametoa risiti kwa usahihi hakuna shida haitofautiani na mtu ambaye anasimamishwa na trafiki, trafiki akikagua kama una leseni anakuruhusu unaondoka kama huna atachukua hatua,” amesema.

Akizungumzia kuhusu sheria mpya ya usajili wa stoo ambayo imelalamikiwa pia na wafanyabiashara hao, amesema sheria hiyo imetungwa na bunge ambayo inawataka wenye stoo na mabohari kusajili na kupeleka marejesho ya kila mwezi ili kuonesha kiasi cha mzigo kilichopo, kilichoingia na killichotoka ili kuwa na mlinganyo ulio sahihi.

TPA yakanusha madai ya urasimu Bandari ya Dar es Salaam

“Kama unavyofahamu biashara sasa hivi mwingine anakuwa na fremu lakini biashara inafanyika ‘godown’ na huku ndo kunatokea changamoto kwa sababu kama ana duka dogo tu lakini mzigo mkubwa uko kwenye godown, huwezi kujua kiasi gani kinatoka kwenye godown wakati mwingine hata risiti hazitolewi na wakati mwingine risiti ikitolewa inatolewa risiti moja na inasindikiza mzigo kutwa,” ameeleza.

Aidha, kuhusu suala la rushwa linalodaiwa kufanyika wakati wa ukamataji amewataka kufikisha malalamiko hayo katika mamlaka husika ambayo ni Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) ili hatua stahiki zichukuliwe pamoja na kuwataka wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao kwa kutunza kumbukumbu kwa usahihi ili kuepusha kuleta ushawishi.

Send this to a friend