Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 22.28 ikiwa ni sawa na ufanisi wa asilimia 99.22 ya lengo la makusanyo ya shilingi trilioni 22.45 katika kipindi cha mwaka wa Fedha (Julai- Juni) 2021/2022.
Makusanyo hayo ni ongezeko la shilingi trilioni 4.13 ikilinganishwa na kiwango cha makusanyo cha shilingi trilioni 18.15 kilichofikiwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2020/2021, ambapo ongezeko hilo ni sawa na ukuaji wa makusanyo kwa asilimia 22.77.
TRA imesema ufanisi huo wa kiutendaji ni matokeo ya kuendelea kuimarika kwa matumizi ya mifumo ya kielekroniki katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi, mazingira ya ufanyaji biashara nchini na mwenendo wa ulipaji kodi kwa hiari.
Matokeo mengine ni uboreshwaji wa mahusiano kati ya TRA na walipa kodi, utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya Mahakama na kuongezeka kwa kiwango cha uhamasishaji na utoaji elimu kwa mlipakodi kwa njia mbalimbali.