TRA yafunga akaunti ya Shule ya St. Jude, wanafunzi wasimamishwa

0
32

Wanafunzi wanaopatiwa ufadhili wa masomo katika shule St. Jude mkoani Arusha wamesimamishwa masomo baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufungia akaunti za mfadhili wao, jambo lililosababisha shule kushindwa kujiendesha ikiwemo kuwahudumia watoto.

Hatua hiyo imepelekea wazazi wa watoto hao mkoani humo kuandamana kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kulalamikia hatua hiyo iliyopelekea watoto wao kusimamishwa masomo kwa wiki mbili sasa.

Aidha, wazazi hao wamedai kuwa TRA imechukua fedha kutoka kwenye akaunti ya shule na kusababisha kushindwa kujiendesha.

Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha, John Mwigura amesema mamlaka hiyo inadai malimbikizo ya kodi ya muda mrefu. Ameongeza kuwa awali shule hiyo ilikataa kulipa kwa maelezo kuwa haifanyi biashara na hivyo kufungua kesi Mahakama ya Rufaa ambayo ilitoa uamuzi na kuitaka St. Jude kulipa kodi hiyo.

Shule hiyo ya mchepuo wa Kiingereza inatoa ufadhili kwa wanafunzi 1,800 katika ngazi ya msingi na sekondari nchini. Pia, inawasaidia wahitimu wake katika ngazi ya elimu ya juu nchini.

Send this to a friend