Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 (Julai hadi Septemba) imekusanya shilingi trilioni 6.58, sawa na ufanisi wa asilimia 97.53 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 6.75.
Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 11.05 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi trilioni 5.92 yaliyofikiwa katika kipindi kama hiki katika mwaka 2022/23.
Aidha, TRA imesema katika kipindi cha Septemba 2023 imekusanya shilingi trilioni 2.63 ikiwa ni ufanisi wa asilimia 108.41 ya lengo la kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 2.42 ambapo makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 15.49 ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.27 kilichokusanywa katika mwaka wa fedha 2022/23.
TRA imebainisha kuwa mafanikio yaliyofikiwa ni matokeo ya hatua mbalimbali zikiwemo miongozo mbalimbali inayotolewa na Rais Samia Suluhu, kuongezeka kwa uwekezaji na ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongezeka kwa matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika usimamizi wa kodi na kuongezeka kwa hamasa kwa wananchi kuhusiana na masuala ya kodi.