Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, mwaka wa fedha 2024/25 imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 7.79 sawa na ufanisi wa asilimia 104.9 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 7.42.
Katika taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo imesema makusanyo hayo ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 18.4 ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa mwaka 2023/24 ni kiwango cha juu ambacho hakijawahi kufikiwa na TRA kwa miezi ya Julai – Setemba ya mwaka wa fedha, sawa na ukuaji wa asilimia 77.4 ukilinganisha na makusanyo ya kipindi kama hicho mwaka 2020/21.
Kadhalika, TRA imesema katika kipindi cha mwezi Septemba mwaka wa fedha 2024/25 imefanikiwa kukusanya shilingi trilioni 3.02 sawa na ufanisi wa asilimia 105 ya lengo la kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 2.88, makusanyo ambayo pia ni kiwango cha juu cha ukuaji wa asilimia 77.6 kuweza kukusanywa katika mwezi Septemba ndani ya miaka mitano, tangu mwaka 2020/2021.
Aidha, TRA imesema kuongezeka kwa mapato hayo kunachangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa vitendo maelekezo ya Rais Samia Suluhu ya kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari, kukua kwa ushirikiano na mahusiano mazuri kati ya TRA na walipa kodi wote nchini, utoaji wa huduma bora kwa walipa kodi, utendaji kazi mzuri na kijituma kwa watumishi.
Sababu zingine ni kuongezeka kwa usimamizi wa wafanyakazi kwa kukemea vitendo vya uvunjifu wa maadili ikiwemo rushwa na kuchukua hatua kwa wanaothibitika kuhusika katika vitendo hivyo, kuendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji na kutengeneza mfumo wa kurahisisha ugomboaji wa mizigo inayoingia kwa utaratibu wa ufungishaji wa mizigo (consolidation).