TRC kuajiri wafanyakazi 2,460 mradi wa SGR Dar es Salaam – Makutupora

0
141

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetangaza mpango wa kuajiri wafanyakazi 2,460 chini ya mradi wa reli ya kisasa (SGR), unaojumuisha sehemu mbili kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora.

Hatua hiyo inakuja baada ya ajira 115,000 kutolewa na wakandarasi wanaofanya kazi katika hatua sita za mwanzo za mradi huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya TRC, ajira hizo zitaendelea kutolewa kwa awamu. Katika mwaka wa fedha wa 2024/25, zaidi ya wafanyakazi 500 wameajiriwa, huku mwaka wa sasa wa fedha 2025/26, wafanyakazi 272 wengine wanatarajiwa kuajiriwa. Mchakato huu utaendelea hadi nafasi zote 2,460 zitakapojazwa.

Shirika limeeleza kuwa ajira 115,000 zilizotokana na wakandarasi, zimewafaidisha Watanzania wenye ngazi mbalimbali za elimu, kuanzia waliomaliza shule ya msingi hadi wale wenye ujuzi maalum katika nyanja mbalimbali.

“Kwa ufafanuzi, kati ya idadi hiyo, 35,000 ni ajira za moja kwa moja, huku zaidi ya 80,000 zikichangia ajira zisizo za moja kwa moja. Hizi ni pamoja na fursa kwa wauzaji wa chakula, waendesha bodaboda na bajaji, pamoja na watoa huduma za mawasiliano ya simu na uhamishaji wa fedha,” imesema taarifa hiyo.

Mradi wa SGR umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa ajira na maendeleo ya uchumi, huku ukiimarisha miundombinu ya usafirishaji wa reli nchini Tanzania.

Send this to a friend