TRC: Kusimama kwa treni ya mchongoko ilikuwa ni hujuma

0
61

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeutaarifu umma kupuuza taarifa zinazosambazwa na baadhi ya watu kuhusu kusimama kwa treni za EMU, Electric Multiple Unit (mchongoko) pamoja na changamoto za umeme, ikisema kuwa haijawahi kuwa na changamoto za umeme tangu kuanza kwa safari hizo Juni 14, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na TRC imeeleza kuwa kilichotokea Novemba 3, mwaka huu na kusababisha kusimama kwa treni ya EMU kwa takriban saa 6 ni hujuma kutokana na kukatika ama kukatwa kwa nyaya (catenary) zinazochukua umeme kutoka njia ya umeme kupeleka kwenye treni.

“Shirika la Reli Tanzania linauhakikishia umma kuwa hakuna treni ya mchongoko iliyopata hitilafu ya kiufundi. Tayari baadhi ya wahusika wamekamatwa na hatua stahiki dhidi yao zimeshaanza kuchukuliwa ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo husika,” imeeleza taarifa.

Aidha, TRC imesema inawakumbusha wananchi kuwa bado iko kwenye kipindi cha mwaka mmoja cha matazamio, na endapo kutakuwa na changamoto zozote zitakazojitokeza shirika hilo litaujulisha umma kwa uwazi kama linavyofanya siku zote kupitia vyanzo vyake rasmi vyake rasmi.