Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka kutakuwa na ongezeko la safari za treni kuelekea mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, na Arusha.
Taarifa iliyotolewa na Shirika hilo imesema siku ya Jumatano itaongezeka kujumuisha siku ya Jumatatu na Ijumaa, hivyo kufanya jumla ya safari tatu kwa juma kuelekea mikoa hiyo.
“Ongezeko hilo la siku ya Jumatano ni hatua mahususi za TRC kukabiliana na ongezeko la abiria katika kipindi hiki, hususani kuelekea mikoa ya Kaskazini Mashariki mwa Tanzania,” imesema.
Aidha, TRC imesema kila siku ya Jumatatu ya juma kuanzia Desemba 9, mwaka huu mpaka mwanzoni mwa Januari, 2025 Shirika litakuwa likipeleka mabehewa 18 yatakayobeba abiria takriban 1000 mpaka 1200 kwa wakati mmoja kuelekea mikoa hiyo.
Wakati huo huo, TRC imewahakikishia wateja kuwa hakutakuwa na ongezeko la nauli katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka.